Mwanaume mmoja raia wa Pakistani mwenye uhusiano na Iran ameshtakiwa kwa madai ya njama ya kumuua Donald Trump na wanasiasa wengine wa Marekani.
Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray aliuita mpango huo “njama hatari ya kuua kwa kukodisha.
Asif Merchant, mwenye umri wa miaka 46, anashtakiwa kwa kujaribu kuajiri mshambuliaji huko New York ili kuwaua maafisa mashuhuri wa Marekani.
Merchant alikamatwa mwezi Julai na anazuiliwa mjini New York. Kulingana na mashtaka ya wizara ya sheria, Bw Merchant aliwasili Marekani kutoka Pakistan mwezi Aprili baada ya kukaa kwa muda nchini Iran.
Baada ya kufika, inadaiwa aliwasiliana na mtu ambaye aliamini angeweza kusaidia mpango wa mauaji.
Inadaiwa kuwa Merchant alimwambia mtu ambaye alipanga kuondoka Marekani kabla ya walengwa kuuawa, na kwamba angewasiliana kwa kutumia maneno ya siri.