Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International, limesema Serikali ya Ethiopia inashindwa kuzuia vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu kwenye maeneo yenye mizozo, wakati huu pia shirika jingine la Human Rights Watch likilaani kushikiliwa kinyume cha sheria kwa kaka wa mwanasiasa wa upinzani aliyeuawa hivi karibuni.
Amnesty inasema licha ya kumalizika kwa vita iliyodumu kwa miaka miwili kwenye eneo la kaskazini la Tigray mwezi Novemba mwaka 2022, bado taifa hilo linashuhudia mizozo ikiwemo katika mikoa ya Amhara na Oromia.
Katika taarifa yake, Amnesty imesema bado vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinashuhudiwa huko Amhara, Tigray na Oromia, huku wahusika wakiachwa bila kuchukuliwa hatua.
Aidha shirika hilo limesema, matamshi ya waziri mkuu Abiy Ahmed, kuwa jeshi la nchi yake halijatekelkeza vitendo vyovyote vya ukiukaji wa haki za binadamu, yanaonesha wazi namna serikali imeendelea kufumbia macho vitendo hivyo.
Katika hatua nyingine, shirika la Human Rights Watch, limezitaka mamlaka za Ethiopia kuwaachia huru watu 11 akiwemo kaka wa mwanasiasa Bate Urgessa, kiongozi wa vuguvugu la Oromia aliyeuawa mwezi Aprili mwaka huu.