Maelfu ya polisi wa kutuliza ghasia nchini Uingereza siku ya Jumatano walisimama tayari kukabiliana na zaidi ya machafuko, ambayo yalizuka zaidi ya wiki moja iliyopita baada ya watoto watatu kuuawa.
Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yamepanga maandamano katika maeneo zaidi ya 30, huku mawakili wa uhamiaji na majengo yanayowakaribisha wanaotafuta hifadhi yakiwekwa kuwa shabaha kuu, kulingana na machapisho kwenye programu ya kutuma ujumbe Telegram iliyovuja kwa vyombo vya habari vya Uingereza.
Serikali imesema polisi maalum 6,000 wako tayari kukabiliana na machafuko mabaya zaidi nchini Uingereza katika kipindi cha muongo mmoja, ambao umeshuhudia mamia wakikamatwa na zaidi ya 100 kushtakiwa.
Vurugu hizo zilizuka baada ya wasichana watatu, wenye umri wa miaka tisa, saba na sita, kuuawa na watoto wengine watano kujeruhiwa vibaya wakati wa shambulio la kisu kwenye darasa la dansi la Taylor Swift huko Southport, kaskazini magharibi mwa Uingereza.
Hapo awali uvumi wa uwongo ulienea kwenye mitandao ya kijamii ukisema mshambuliaji huyo alikuwa Muislamu anayetafuta hifadhi. Mshukiwa huyo baadaye alitambuliwa kama Axel Rudakubana mwenye umri wa miaka 17, mzaliwa wa Wales. Vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuwa wazazi wake wanatoka Rwanda.
Licha ya taarifa hiyo ya polisi, ghasia za awali huko Southport zilijikita karibu na msikiti wa eneo hilo, na vurugu zilizoenea zimetikisa Uingereza na Ireland Kaskazini tangu wakati huo.