Mtu anayetarajiwa kuwa mgombea urais nchini Tunisia amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, na hivyo kuashiria kikwazo kingine kwa upinzani changa nchini humo kumpinga Rais Kais Saied anapowania muhula mpya.
Abir Moussi, wakili mwenye umri wa miaka 49 na mkuu wa chama cha mrengo wa kulia cha Free Destourian Party, alikamatwa mwezi Oktoba baada ya kukosoa mchakato wa uchaguzi na amri za rais zinazouongoza, akidai kukosekana kwa uwazi.
Kufuatia malalamishi ya halmashauri ya kusimamia uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Kaskazini, alipatikana na hatia ya kukiuka amri yenye utata ya kupinga habari ghushi iliyoharamisha kueneza habari zinazokashifu au kuwadhuru wengine.
Sheria hiyo imekuwa ikitumika sana kuwashtaki wale wanaokosoa mamlaka.
Wakili wa Moussi Nafaa Laribi aliambia The Associated Press Jumanne kwamba bado ana nia ya kugombea katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 6, na kwamba, tofauti na wagombea wengine, hakuna chochote katika hukumu ya Jumatatu kinachomzuia kugombea.
Laribi alisema morali ya Moussi imesalia kuwa juu, na alipanga kukata rufaa.
Hukumu hiyo ni ya hivi punde zaidi katika msako mkali ambao waangalizi wa mambo wamesema umechochewa kisiasa dhidi ya wakosoaji wa Saied, bila kujali misimamo ya kisiasa.