Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amepata uungwaji mkono wa chama chake kugombea muhula wa pili katika uchaguzi wa mwaka ujao, lakini nafasi yake ya kubakia madarakani inaweza kutegemea chama chake cha Malawi Congress Party kupata mshirika imara wa muungano.
Malawi Congress Party, ambayo ilikuwa katika muungano wa uchaguzi na Vuguvugu la Mabadiliko la Umoja tangu 2020, sasa haina mshirika mkubwa baada ya UTM kusema kwamba itaondoa ushirikiano huo baada ya kifo cha Makamu wa Rais wa zamani Saulos Klaus Chilima katika ajali ya ndege mwezi Juni. .
Chilima alikuwa kiongozi wa UTM na chama chake kilimsaidia Chakwera kupata kura nyingi katika uchaguzi wa 2020. Mfumo wa kisiasa wa Malawi unahitaji mgombea urais kupata zaidi ya 50% ya kura ili kutangazwa mshindi.
Chakwera aliwaambia wajumbe katika kongamano la MCP lililoidhinisha azma yake ya kuwania muhula wa pili kwamba anaamini uungwaji mkono kwa chama chake umeongezeka tangu uchaguzi uliopita.
“Hili si kongamano la kawaida kwa sababu ni kongamano la chama litakaloshinda 2025,” Chakwera alisema katika hotuba yake Alhamisi.