Wananchi wengi wamejitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo limekamilika leo tarehe 11 Agosti, 2024 mkoani Geita baada ya kufanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 05 Agosti, 2024.
Mwandishi wetu, ameshuhudia uwepo wa wananchi wengi vituoni haswa vijana ambapo kwenye baadhi ya maeneo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ililazimika kuongeza vifaa na watendaji.
Wakizungumzia mwenendo wa zoezi hilo Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Geita Mji, Bw. Yefred Mnyenzi na Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Sarah Yohana wamesema wengi waliojitokeza ni vijana ambao wanajiandikisha kwa mara ya kwanza.
“Kwa siku hawapungui wapiga kura 10,000 ambao wamejitokeza, kati yao wapiga kura wapya ambao wengi ni vijana ni kama 8,000 kwa siku, kwa ujumla nawapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi,” amesema Bw. Myenzi, Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Geita Mji.
Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Sarah Yohana amesema “Wananchi wamejitokeza kwa wingi haswa vijana, maeneo yaliyokuwa na wananchi wengi zaidi ni ya Katoro, Rwemgaza na Kiziba ambapo tumeongeza vifaa na watendaji wa vituo, kwa mfano, Katoro tumeongeza BVR Kits 10 na Waandikishaji na Waendesha Vifaa vya Bayometriki 20”.
Wakizungungumza kwa nyakati tofauti wapiga kura waliojiandikisha na kuboresha taarifa zao wameishukuru INEC kwa kuboresha huduma kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ambayo imerahisisha zoezi hilo jambo ambalo limepunguza muda wa kujiandikisha na kuboresha taarifa ambapo wameweza kupata kadi zao ndani ya dakika tatu hadi tano.
“Kwa mara ya kwanza nimeweza kupata kadi yangu hii ya mpiga kura, ambayo itaniwezesha kupiga kura kumchagua kiongozi wangu. Nashukuru kwa teknolojia iliyowekwa nimeweza kutumia takribani dakika nne hadi kupata kadi yangu ya mpiga kura,” amesema Angel Lema ambaye amefikisha miaka 18 mwaka huu.