Takriban miaka mitatu baada ya kuungana tena kwa kundi maarufu kutoka nchini Nigeria P-square, mapacha wawili wanaounda kundi hilo Peter na Paul Okoye wametengana kwa mara nyingine tena. Katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni na redio ya City FM nchini Nigeria Paul Okoye al maarufu kama Rude Boy alifichua kuwa ameachana na pacha wake akiongeza kuwa Peter alisema kuwa hana hamu tena na kundi hilo.
Mapya yameibuka mapema hii leo baada ya Peter wa P-Square ku-post barua nzito kupitia ukurasa wake wa Instagram iliyoelekezwa kwa kaka yake akilalamika kuwa anamdharau na pia anatumia nguvu nyingi kwenda kwenye vyombo vya habari akisema hakuwa na mchango wowote mkubwa katika uandishi wa nyimbo nyingi zilizofanya vizuri walipokuwa katika kundi moja huku nyimbo waliomshirikisha staa kutoka nchini Marekani TI ambayo aliandika ilifanya vibaya pia alimshtumu kaka yake kusambaza habari za kuwa yeye ndie “mtunzi wa nyimbo, mtayarishaji, mwimbaji na director wa video zote za kundi la P-SQUARE, ikijumuisha kila kitu pamoja na mkurugenzi wa video, bendi, promota, meneja, hata mwandishi wa choir wa kundi hilo na kwamba asilimia 99% ya kazi zote za muziki zilikuwa za kwake.”
Barua yenye kurasa nne aliyoandikiwa “Rude boy” pia imebeba migogoro ya familia ambapo Peter alisema “Mara nyingi huwa najiuliza, unafaidika nini kwa kunidharau kila wakati, Umemkosea heshima mke wangu, umeivunjia heshima familia yangu, umeidharau talanta yangu, maoni yangu na hata kumuunga mkono adui alipokuwa akijaribu kunidhulumu.
Sasa, kwa sasa umeamua kujaribu kuwageuza mashabiki wote dhidi yangu na kuwafanya waamini kuwa nakuonea wivu. Umekuwa ukifanya kila kitu ili mashabiki wanichukie lakini Hawatanichukia kamwe; badala yake watatuchukia wote kwa sababu tumewakatia tamaa na kuwavunjia heshima. Natumai umefurahi sasa. Sikutakii chochote zaidi ya yote yaliyo mema kaka Ama wote wale wanaoamini uwongo na simulizi zote za uwongo kwa kusema Tafadhali niruhusu nifanye muziki wangu kwa amani.”
P-square ni kundi linalojulikana kwa kuliteka soko la Africa kwa miaka kadhaa sasa baada ya kutoa ngoma kali kama
“Do me” “Alingo” “Beautiful Onyinye” na ngoma nyingi zilizofanya vizuri sana duniani, ila hivi karibuni wawili hao wameonekana wakiendeleza kazi zao za muziki kama wasanii wa kujitegemea, ambapo Mr P alitamba na ngoma ya ‘Kisela’ aliyoimba na msanii Vanessa Mdee huku ‘Rude Boy’ akiimba na Ali Kiba “Salute” nchini Tanzania. Kundi hili lilitengana kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na kurudiana 2021.