Kiongozi wa kanisa lililosababisha waumini wake kufunga hadi kufa nchini Kenya Paul McKenzie amekana mashtaka ya Mauaji ya kutokusudia kufuatia vifo vya waumini zaidi ya 400 katika mkasa unaohusiana na ibada katika pwani ya Kenya.
McKenzie pamoja na washukiwa wengine 94, walifikishwa mahakamani mjini Mombasa leo siku ya Jumatatu na kukanusha mashtaka.
Mchungaji huyo na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka mengi ya kuua bila kukusudia katika mauajiambayo yamepatiwa jina la mauaji ya Shakahola.
McKenzie ambaye alikamatwa Aprili iliyopita, baada ya miili kugunduliwa katika Msitu wa Shakahola, anatuhumiwa kuwahimiza wafuasi wake wafe kwa njaa ili “kumlaki Yesu,” habari iliozua mshtuko mkubwa nchini Kenya na kote duniani.
Mwendesha mashtaka Alexander Jami Yamina amesema kuwa kesi hiyo ni ya kipekee nchini Kenya, na washukiwa watashtakiwa chini ya sheria inayohusiana na makubaliano ya kujitoa uhai.
Mackenzie amefikishwa mahakamani jijini Mombasa akiwa pamoja na washukiwa wengine 94 kwa mujibu wa mwendesha na maofisa wa mahakama.
“Hakujatokea kesi nyengine ya mauaji kama hii nchini kenya,” mwendesha mashtaka Alexander Jami Yamina amewaambia wanahabari, akiongeza kwamba watashtakiwa kwa mujibu wa sheria za Kenya.
Takriban mashahidi 420 wameandaliwa na upande wa mashtaka huku kesi hiyo ikipangwa kuendelea kwa siku nne hadi Alhamisi.
Washukiwa hao, 55 wakiwa ni wanaume na 40 wakiwa ni wanawake walifunguliwa kesi ya ugaidi mwezi uliopita ambapo pia wanakabiliwa na mashtaka mengine ikiwemo mauaji, kuwatesa watoto, makosa ambayo waendesha mashtaka wanasema yalifanyika kati ya mwaka wa 2020 hadi 2023.
Mwezi Machi mwaka huu, mamlaka ilianza kutoa miili ya baadhi ya waathiriwa kwa ndugu zao baada ya miezi kadhaa ya kazi kubwa ya kuwatambua kwa kutumia chembechembe za DNA na hadi sasa milii 34 imerejeshwa.
Tayari miili ya watu 440 imefukuliwa kutoka kwa makaburi ya pamoja katika msitu huo.
Mackenzie alikuwa ameanzisha Kanisa lake la Good News International Church mwaka wa 2003, lakini akasema alilifunga mwaka wa 2019 na kuhamia Shakahola kujiandaa na kile alichotabiri kuwa mwisho wa dunia Agosti mwaka jana.