WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Selemani Jafo ameiagiza Tume ya Ushindani nchini (FCC) kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu mikataba baina ya wawekezaji wazawa na wageni mara baada ya kubaini kuwa makampuni kutoka nje kuingia mikataba kinyume na utaratibu hususani kwenye Sekta ya Madini jambo ambalo linapelekea kuporwa vitalu vyao na mabilioni ya fedha kwenda nje ya nchi na Wawekezaji wa Tanzania kubaki maskini.
Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Selemani Jafo wakati alipofanya ziara kwenye ofisi za FCC ikiwa ni siku yake kwanza tokea alipoteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri kwenye wizara hiyo huku akisisitiza Taasisi hiyo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa sababu Serikali na Watanzania wanawategemea katika kuhakikisha Sekta nzima ya biashara inakuwa na kuleta tija.
Kwa upande wao Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC) Dkt. Aggrey Kalimwage Mlimuka na Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bw. William Erio wamesema kuwa wamepokea maagizo hayo katika kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo na kuendelea kurekebisha sheria ambazo zitakuwa na faida kwa pande zote mbili ili kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na kuvutia wawekezaji.