Mwandishi wa habari wa Uingereza, JK Rowling na bilionea wa Marekani, Elon Musk wametajwa katika kesi ya unyanyasaji mtandaoni iliyofunguliwa na bondia bingwa wa Olimpiki kutoka nchini Algeria, Imane Khelif aliyefeli vipimo vya jinsia.
Khelif ambaye alishinda medali ya dhahabu akiiwakilisha nchi yake katika taji la kilo 66 kwa wanawake, na kuzua mjadala mkali kuhusu jinsia yake na ushiriki wake katika michezo ya Olimpiki licha ya kufeli vipimo vya jinsia mwaka jana.
Usiku wa kuamkia leo Jumatano, Agosti 14, 2024 wakili wa Khelif, Nabil Boudi, alifichua kwamba Rowling na Musk wote wametajwa katika malalamiko ya jinai ambayo bondia huyo amewasilisha kwa mamlaka za kisheria nchini Ufaransa.
“JK Rowling na Elon Musk wametajwa katika kesi hiyo.” ameongeza kuwa Donald Trump pia atakuwa sehemu ya uchunguzi wa ofisi ya mwendesha mashtaka huko Paris, kesi hiyo inadai kuwa Khelif alikumbwa na “unyanyasaji uliokithiri wa mtandaoni.”
Bondia huyo anadai kuwa ameathiriwa na unyanyasaji mtandaoni kutoka kwa watu hao waliomfanyia “unyanyasaji wa kijinsia, ubaguzi wa rangi na kijinsia”, ambao wakili wake ameuelezea kama “unyanyasaji wa kidijitali”.
Mualgeria huyo aliteka baadhi ya vichwa vya habari vikubwa vya Olimpiki ya 2024 baada ya kumshinda bondia wa Italia, Angela Carini ndani ya sekunde 46 kwenye pambano lao, bondia huyo alilia na kukataa kumpa mkono Khelif.