Mshindi wa kwanza wa medali ya dhahabu wa mashindano ya Olimpiki nchini Botswana, Letsile Tebogo amekaribishwa nchini humo kifalme, Jumanne, Agosti 12, 2024 kwa shangwe na maelfu ya watu waliojaza uwanja wa taifa hilo kusherehekea na kumuenzi mwanariadha huyo.
Baada ya kufika mji mkuu wa Gaborone, Tebogo alisindikizwa kwa basi kubwa lenye paa la wazi kwa ajili ya gwaride la wanariadha ambapo mashabiki walijaa, wakimshangilia na kupeperusha bendera ya taifa hilo yenye rangi ya bluu na nyeusi.
Tebogo, 21, alishinda medali ya dhahabu ya kwanza kabisa ya Olimpiki ya Botswana Agosti 8, 2024 baada ya kuwaacha nyuma Kenny Bednarek wa Marekani na Noah Lyles katika mbio za mita 200 kwenye michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Mwanariadha huyo ameweka rekodi ya kuwa mwafrika wa kwanza kushinda mbio za mita 200 kwa wanaume kwenye michezo hiyo, akifanya hivyo katika rekodi ya sekunde 19.46 , kisha akashinda medali ya fedha katika mbio za kupokezana za mita 4×400 wanaume.