Afisa wa polisi huko Ohio ameshtakiwa kwa mauaji baada ya kumpiga risasi mwanamke mjamzito, Ta’Kiya Young, 21, ambaye alikuwa na ujauzito wa takriban wiki 25, aliuawa mwaka jana, pamoja na binti yake aliyekua tumboni katika tukio hilo.
Mahakama kuu ya Columbus imetangaza rasmi Jumanne wiki hii, Agosti 13, 2024 kupata ushahidi wa kutosha kumshtaki afisa wa polisi wa Blendon Township, Connor Grubb kwa mauaji, kuua bila kukusudia, na shambulio la kudhuru.
Picha za kamera katika tukio hilo, zilizotolewa mwaka jana, zilionyesha polisi wakijaribu kumzuia Bi Young asiendeshe gari ili waweze kumhoji kuhusu kesi ya wizi, afisa Grubb alifyatua risasi huku akimuamuru atoke nje ya gari.
Wadadisi wanasema Bi Young alishutumiwa kuiba pombe dukani katika duka la vyakula la Kroger, hata hivyo mawakili wa afisa Grubb wanasema kuwa afisa huyo alijitetea, wakidai kuwa video hiyo inamwonyesha akigongwa na gari la Bi Young.
Mkuu wa polisi wa Blendon Township, Ohio nchini Marekani, John Belford amesema idara yake imeanza kuchukua hatua za kinidhamu kwa Grubb baada ya kushtakiwa, afisa huyo atafikishwa kortini tena leo Jumatano, Agosti 14, 2024 saa moja jioni kwa saa za huko.