Mwenyekiti wa Jumuiya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa Mary Chatanda, ameendelea kukemea vikali vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto, huku akisisitiza mapambano dhidi ya kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia nchini.
Akiwa Jijini Mwanza Mwenyekiti huyo wa (UWT) Taifa, katika uzinduzi wa Kamati inayolenga Mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia (UWT), mkoa wa Mwanza ameeleza kuwa kwa sasa hali ni mbaya kutokana na vitendo vya ulawiti na ubakaji kushamiri kwa baadhi ya maeneo nchini, sambamba na kuwataka wazazi kutofumbia macho vitendo hivyo pale inapobainika ndugu wa karibu kuhusika.
Mwenyekiti huyo amekwenda mbali zaidi na kuwataka wanafamilia kuwa makini inapotokea wametembelewa na wageni majumbani wasiruhusu kulala nyumbani na badala yake, wawapeleke nyumba za kulala wageni, huku akisema atawashawishi Wabunge wanawake kupitisha sheria ya wanaume kuhasiwa pale inapobainika kutenda vitendo hivyo.
Halima Nassor ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mapambano dhidi ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia (UWT) mkoa wa Mwanza, anaweka bayana dhamira yao ya kutaka kuzifikia wilaya zote za Mwanza, huku akibainisha takwimu za ukatili wa kijinsia mkoa wa Mwanza.
Uzinduzi wa Kamati ya Mapambano dhidi ya kupinga Ukatili umefanyika Jijini Mwanza, ikiwa na kauli mbiu isemayo ‘Vunja minyororo ya Ukatili wa Kijinsia, Mwanza salama’.