MKURUGENZI wa Shirika la WaterAid, Ana Mzinga, amesema bado ipo changamoto ya upatikanaji wa maji hasa katika zahanati na vituo vya kutoa huduma za afya vilivyojengwa jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi nchini.
Mzinga aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam Agosti 14,2024 wakati wa uzunduzi wa mkakati wa Shirika la Water Aid kwa kuwashirikisha wadau wa maji na usafi wa mazingira (WASH).
“Tumeona kuna vituo vya afya ambavyo vinaonyesha huduma za maji na usafi wa mazingira hazijafika hili tunaliona ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa pamoja ndio maana tumeamua kuanzisha mpango mkakati wa kuonyesha maeneo ambayo tunaweza kufanya kazi ili kuwasogezea huduma za maji hasa katika vituo vya afya na shule zetu,”alisema Mzinga.
Alisema kutokana na changamoto hiyo wameona athari kubwa inaenda kwa mwanamke ama kwa mtoto wa kike kutokuwepo kwa asilimia 100 ya maji na usafi wa mazingira inachangia kuwarudisha nyuma wanawake kiuchumi .
Aidha, alisema mpango mkakati huo waliouanzisha wamejipanga katika kuleta taarifa rasmi ni wapi ambapo kunahitajika kufanyiwa kazi na kuwekeza zaidi kufanya utafiti na kufuatilia maeneo ambayo yanahitaji kuwekwa kipaumbele na kuunganisha wadau ili kupanga kwa pamoja katika kutekeleza mkakati huo.
Naye Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangalla amewataka wadau wa maji na usafi wa mazingira kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa sera na mipango yake ili kuwezesha utoaji wa huduma ya maji na usafi katika jamii.
Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanaopiga vita Usugu wa Dawa Tanzania (uvida) alisema licha ya Tanzania kuwa na sera na mipango mizuri, hakuna utekelezaji.
Alisema kupitia mkutano huo, wadau waazimie kuweka mikakati ya kufanikisha mipango iliyowekwa.
“Kwanza ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fedha za kutosha kwenye miradi ya maji na usafi wa mazingira kwa ujumla wake na pili ni kuhakikisha wadau wote wanakuja pamoja kusukuma ajenda hiyo ya mazingira kwa lengo la kumpa kipaumbele mwanamke,”alisema na kuongeza kuwa;
Awali akitoa mada katika mkutano huo, Mkuu wa kitengo cha sera na ushawishi kutoka WaterAid, Christina Mhando, alisema hadi mwaka 2021 vyanzo vinaonyesha kulikuwa na takribani vituo vya afya 8,549 zikiwemo zahanati 7,200 ambazo na asilimia 74 zinamilikiwa na serikali.
Alisema karibu nusu ya vituo hivyo havina maji ya bomba na hata vilivyounganishwa na maji ya bomba havipati maji ya uhakika.
Alisema hali hiyo inawaathiri watoa huduma walio mstari wa mbele kama wauguzi, wakunga na wanawake wakati wa kujifungua na wagonjwa wengine.
Naye Muuguzi na Mkunga wa kituo cha afya cha Msanga Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Robart Mgema, alisema awali walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kituoni hali iliyowalazima wakina mama kuja na maji kwenye kituo cha afya wanapotaka kutibiwa.
Alisema kwa sasa wanashukuru kupatiwa mradi wa maji na shirika la WaterAid hali ambayo imewanufaisha wanawake kupata huduma sahihi katika mazingira bora.
“Uwepo wa mradi wa maji katika mazingira ya kutoa huduma za afya ni chanzo cha utoaji wa huduma bora yanapokopasekana maji wakina mama wanapata chanagmoto nyingi ikiwemo magonjwa ya maambukizi,”alisema.