Bunge la Thailand limemchagua Paetongtarn Shinawatra, binti wa bilionea na kiongozi wa zamani Thaksin, kuwa waziri mkuu.
Akiwa na umri wa miaka 37, atakuwa Waziri Mkuu mdogo zaidi nchini na mwanamke wa pili katika wadhifa huo, baada ya shangazi yake Yingluck.
Uteuzi wake umefanyika siku mbili tu baada ya Waziri Mkuu wa zamani Srettha Thavisin kufutwa kazi na mahakama ya kikatiba.
Wote wawili wanatoka chama cha Pheu Thai, ambacho kilishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa 2023 lakini wakaunda muungano unaotawala.
Bi Paetongtarn anakabiliwa na kibarua kigumu cha kufufua uchumi uliokwama wa Thailand na kuepuka mapinduzi ya kijeshi na uingiliaji kati wa mahakama ambao umeondoa tawala nne zilizopita zikiongozwa na familia yake.
Bi Paetongtarn, ambaye aliidhinishwa kwa kupata kura 319 dhidi ya 145 siku ya Ijumaa, ni wa nne wa ukoo wa Shinawatra kuwa waziri mkuu katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Wengine watatu, akiwemo babake Thaksin na shangazi yake Yingluck, waliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi au maamuzi ya mahakama ya kikatiba.