Kim Jong-un amepigwa picha akiwa amezungukwa na watoto wadogo wanaolia wakitafuta chakula katika jumba la chakula huko Pyongyang, zaidi ya raia 15,000 wa Korea Kaskazini wamemiminika katika mji mkuu wa nchi hiyo baada ya mafuriko makubwa kuikumba.
Kim amekataa ofa za usaidizi, ikiwa ni pamoja na ile ya rais wa Urusi, Vladimir Putin akisema kuwa serikali yake tayari imechukua hatua za kufanya kazi ya uokoaji, nchi hiyo pia imekanusha kuwa kulikuwa na majeruhi katika mafuriko hayo.
Kiongozi huyo alisafiri hadi maeneo yaliyokumbwa na mafuriko mapema wiki hii kwa treni yake huku gari lake kubwa la kivita likiwa ndani yake, picha zilizopigwa Pyongyang siku ya Alhamisi, Agosti 15, 2024 zilionyesha Kim akilakiwa na umati wa watu huku akizuru maeneo ya makaazi ya wale waliotoroka mafuriko.
Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini limesema maelfu ya waathiriwa walisafiri hadi Pyongyang kutoka maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika majimbo ya Pyongan Kaskazini, Jagang na Ryanggang kukwepa mafuriko makubwa yaliyoikumba nchi hiyo mwezi huu.
Ripoti kutoka Korea Kusini zinasema kwamba idadi ya waliofariki au kupotea inaweza kuwa 1,500, inadhaniwa kuwa zaidi ya nyumba 4,000 katika maeneo ya kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo zimeathirika vibaya.