Bilionea wa Nigeria na baba wa msanii Davido, Dr. Deji Adeleke, ametoa mchango wa Naira bilioni 1 (TZS bilioni 1.7) kwa Kanisa la The Eternal Sacred Order of The Cherubim & Seraphim, huko Mount Zion, Surulere, Lagos.
Mnamo Agosti 18, 2024, familia ya Adeleke ilihudhuria ibada ya shukrani katika Jimbo la Lagos kusherehekea maisha ya Nnena Esther Adeleke, ambaye alikuwa mwanzilishi wa kanisa la C&S huko Ede, Jimbo la Osun.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na watu mashuhuri kama vile Gavana wa Jimbo la Ogun, Dapo Abiodun, Gavana wa Jimbo la Lagos, Babajide Sanwo-Olu na Davido.
Katika video inayovuma, Dk. Adedeji Adeleke alisema, “Kwa niaba ya marehemu mama yetu, mama yetu mkubwa marehemu Bi. Esther Adeleke, tunataka kuchangia hazina kiasi cha N1 bilioni.”
Baada ya tamko lake, umati ulilipuka kwa shangwe kubwa, muziki ukapigwa na video nyingine ikimuonyesha Gavana Ademola Adeleke akicheza.
Mchango huo mkubwa wa familia ya Adeleke ulitikisa mitandao ya kijamii, na kusababisha hisia tofauti.