Nchini Mali, imepita miaka minne tangu jeshi lilipochukua uongozi wa nchi hiyo, ambapo wananchi walio wengi wanalalamikia hali ngumu ya uchumi na kukatika kwa umeme kila wakati.
Benki ya dunia kwenye takwimu zake inasema uchumi wa Mali, utashuka kwenye ukuaji wake kutoka asilimia 3.5 hadi 3.1, wakati huu viwango vya umasikini miongoni mwa raia wengi wa Mali, vikiendelea kuongezeka.
Tangu mwezi Agosti mwaka 2020 wakati jeshi lilipochukua madaraka, wananchi wengi wa Mali wanasema bado wanasuburi kuona iwapo maisha yao yataimarika.
Wafanyabiashara wengi wanaotegemea umeme kwa ajili ya kazi zao za kila siku, wanasema miaka minne baadaye, wanaendelea kupata hasara kubwa kwa sababu hahawezi kuendelea na majukumu yao kama zamani kwa ukosefu wa nishati hiyo muhimu.
Mapinduzi nchini Mali, yalichochea mataifa mengine kama Burkina Faso na Niger kufuata mkondo huo na kuondolewa kwa serikali za kiraia, baada ya jeshi kudai kuwa zilishindwa kupambana na utovu wa usalama kutokaana na uwepo wa makundi yanayoshirikiana na Al-Qaeda na Islamic State.