Jeshi la Polisi Tanzania limeomba radhi kwa kila Mtanzania aliyeguswa na kuchukizwa na kauli ya Kamanda wa Polisi Dodoma iliyosambaa kwenye vyombo vya Habari ikiwa na kichwa cha habari “ANAYEDAIWA KUBAKWA NA KULAWITIWA ALIKUWA KAMA ANAJIUZA” na kusema Mkuu wa Jeshi la Polisi amemuhamisha Kamanda huyo kutoka kwenye cheo hiko na kumpeleka Makao Makuu ya Polisi Dodoma huku nafasi hiyo ikichukuliwa na SACP George Katabazi.
Taarifa ya Polisi imesomeka kama ifuatavyo “Tumeona taarifa kwenye Vyombo vya Habari yenye kichwa cha habari kinachosema ‘RPC ANAYEDAIWA KUBAKWA NA KULAWITIWA ALIKUWA KAMA ANAJIUZA’ kauli inayodaiwa kutolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kwenye mazungumzo kwa njia ya simu na Mwandishi wa gazeti la Mwananchi ambaye miongoni mwa maswali aliyomuuliza kamanda (mwandishi huyo), Je upelelezi wa kesi umekamilika? na swali lingine alilomuuliza inadaiwa alikuwa anajiuza? na majibu ya Kamanda aliyomjibu Mwandishi huyo ni kwamba hata kama ni hivyo hangestahili kutendewa hivyo”
“Kauli hiyo kama inavyoonekana kwenye hicho kichwa cha habari siyo msimamo wa Jeshi la Polisi kauli sahihi ni kama zilivyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi kwa umma August 4,6 na 9,2024 na pia kuwa watuhumiwa watafikishwa Mahakamani leo August 19,2024” – imeeleza taarifa.
“Jeshi la Polisi lingependa kuomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye Vyombo vya Habari wakati ufutiliaji ukifanyika kupata usahihi wake, aidha wakati uchunguzi huo wa kupata usahihi wa kauli hizo, Mkuu wa Jeshi la Polisi amefanya mabadiliko madogo kwa kumhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Theopista Mallya kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP George Katabazi”