Kongo itapokea dozi ya kwanza ya chanjo kushughulikia mlipuko wake wa mpox wiki ijayo kutoka Marekani, waziri wa afya wa nchi hiyo alisema siku ya Jumatatu, siku chache baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni kutangaza milipuko ya mpox barani Afrika kuwa dharura ya kimataifa.
Visa vya Mpoksi vimethibitishwa miongoni mwa watoto na watu wazima katika zaidi ya nchi kumi za Kiafrika, na aina mpya ya virusi inaenea. Dozi chache za chanjo zinapatikana katika bara hili.
Kongo ina idadi kubwa ya wagonjwa wa mpox na kwa sasa inahitaji dozi milioni 3 za chanjo.
Marekani na Japan zimejitolea kutoa chanjo, Waziri wa Afya Roger Kamba aliwaambia waandishi wa habari. Hakusema ni dozi ngapi zitatumwa au zile za Japan zingefika lini.