Serikali ya Kenya inalenga kukusanya Dolla za Marekani Bilioni 1.2 kwa kurejesha baadhi ya vipengele vilivyokuwa katika muswada wa fedha wa mwaka wa 2024 uliotupiliwa mbali kutokana na maandamano ya vijana kuupinga.
Rais William Ruto alikuwa ameonya kwamba huenda serikali yake ikikabiliwa na upungufu wa mapato haswa baada ya kuangushwa kwa muswada huo wa fedha.
Muswada huo uliokuwa unalenga kuongeza ushuru kwenye baadhi ya bidhaa, ulipingwa vikali na vijana kupitia maandamano yaliosababisha vifo vya waandamanaji waliopigwa risasi na polisi baada ya kuvamia majengo ya bunge jijini Nairobi.
Katika taarifa yake kupitia televisheni ya ndani (Citizen), Waziri wa mpya wa fehda John Mbadi Jumapili ya wiki iliopita alisema kwamba serikali inawazia kurejesha karibia mikakati 49 ya ushuru ikilenga kukusanya Dolla Bilioni 1.2
Baadhi ya vipengee ambavyo serikali inasema inalenga kuvirejesha kutoka kwenye muswada huo wa fedha uliotupiliwa mbali ni pamoja na, ushuru kwenye baadhi ya bidhaa za kielektroniki pamoja na plastiki, serikali ikisema hatua hiyo inalenga kutunza mazingira.
Baada ya kufutuwa kwa muswada wa fedha wa mwaka wa 2024, ambao kwa mujibu wa serikali, ingesaidia kukusanya karibia Dolla Bilioni 2.7, Rais Ruto alitangaza hatua za kupunguza matumizi ya serikali pamoja na kukopa zaidi ilikuzuia pengo ambalo lilikuwepo.
Kwa mujibu wa runinga ya Citizen, hatua hizo mpya ambazo zipo kwenye muswada huo zinatarajiwa kuanza kutekelezwa kufikia mwisho wa mwezi Septemba.