Polisi katika mji mkuu wa Haiti waliwarushia mabomu ya machozi mamia ya waandamanaji Jumatatu walipotoa wito kwa vyombo vya sheria kuwasaidia kukomesha magenge ambayo yamekuwa yakichukua udhibiti wa vitongoji vyao kwa nguvu.
Waandamanaji walichoma matairi ili kuonyesha hasira yao juu ya hatua ya polisi na kuelezea kufadhaika kwao kwani hatua za hivi majuzi za kumaliza ghasia za magenge huko Port-au-Prince kwa kiasi kikubwa hazijafaulu.
Waandamanaji kama vile mkarabati wa simu mwenye umri wa miaka 24, Marclin Jean-Pierre alisema aliingia barabarani “kuonyesha hasira yangu kwa serikali, ambayo haisikii.”
“Tuko hatarini kwa risasi kurushwa mchana na usiku. Kila mtu anaogopa kutembea nje kwa sababu tutakuwa wahasiriwa wafuatao, “alisema. “Tunawaomba msaada na hawaji.”
Jean-Pierre anaishi katika mtaa wa milimani wa Solino, ambao tangu mwaka jana umekuwa uwanja wa vita kwa magenge yanayotaka kuchukua eneo hilo.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba mashambulizi hayo yalifanywa na muungano wa magenge yanayoongozwa na Kempes Sanon, mteka nyara aliyepatikana na hatia ambaye alitoroka gerezani mwaka wa 2021, na kiongozi wa genge maarufu Jimmy Cherizier, anayejulikana pia kama “Barbecue”.