Jumla ya BVR Kits 4,257 zimesambazwa mkoani Mwanza na Shinyanga kwa ajili ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kufanyika kwenye mikoa hiyo kuanzia kesho tarehe 21 hadi 27 Agosti, 2024.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari amesema hayo mkoani Mwanza leo tarehe 20 Agosti, 2024 na kuongeza kuwa kati ya BVR Kits hizo 3,590 zitatumika vituoni na 667 ni za akiba.
“Jumla ya watendaji 7,562 watahusika katika kuendesha zoezi hilo kwa mikoa hii ya Mwanza na Shinyanga, idadi hiyo inajumuisha Waratibu wa Uandikishaji wa Mikoa, Maafisa Waandikishaji ngazi ya Halmashauri, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Halmashauri, Maafisa Waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata, Waendesha vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi,” amesema.
Ameongeza kuwa kutokana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 400,082 kwenye mikoa hiyo.
“Mkoani Shinyanga wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa ni 209,951 na mkoani Mwanza wapiga kura wapya 190,131 wataandikishwa ambapo kwa ujumla wapiga kura wapya watakaoandikishwa ni 400,082,” amesema.
Ametoa wito kwa wananchi wa mikoa hiyo waliotimiza umri wa miaka 18 na wale watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na wanaohitaji kuboresha taarifa zao kujitokeza mapema na kuacha kasumba ya kusubiri siku ya mwisho.
Uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 ambapo ulienda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi na kufuatiwa na mzunguko wa pili ambao umejumuisha mikoa ya Geita na Kagera.
Kwenye zoezi hilo vituo vya kuandikisha wapiga kura vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.