Meya wa zamani anayeshutumiwa kwa kuwa jasusi wa China na kuwa na uhusiano na makundi ya wahalifu ametoroka kutoka Ufilipino, na kusababisha ghadhabu nchini humo.
Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr alisema Jumatano kwamba “watu watafutwa kazi ” baada ya maafisa kukiri Alice Guo aliondoka nchini bila kutambuliwa mwezi mmoja uliopita na kusafiri hadi Malaysia, Singapore na Indonesia.
Bw Marcos alisema kuondoka kwake “kumeweka wazi ufisadi unaodhoofisha mfumo wetu wa haki na kuondoa imani ya watu”.
Guo hajaonekana tena hadharani tangu mwezi Julai wakati jopo la Seneti lililochunguza madai yake ya kuhusishwa na vituo vya ulaghai na kamali za mtandaoni lilipoamuru akamatwe kwa kukataa kutoa ushahidi wake katika uchunguzi wake.
Anashutumiwa kwa kuruhusu mashirika ya biashara haramu ya binadamu na vituo vya ulaghai kufanya kazi katika mji wake kwa kujifanya kuwa kamali za mtandaoni.
Maseneta pia wamemshutumu kwa kuwa mhudumu au jasusi wa China, wakitaja majibu yake “ya wazi” ya maswali kuhusu asili ya wazazi wake ya China.