Waziri wa Viwanda na Biashara, Suleiman Jafo amesema kuboreshwa kwa huduma za maji na usafi wa mazingira katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani kutasaidia kukuza uchumi na kupunguza magonjwa hatarishi yatokanayo na maji machafu kama vile kuhara.
Jafo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya mradi wa uboreshaji wa tabia za usafi kwenye shule 30 na vituo vya afya 15 katika wilaya ya Kisarawe mradi uliotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Shirika la WaterAid Tanzania uliogharimu zaidi ya Sh. Bilioni nne.
Amesema kuwa upatikanaji wa maji safi, usafi wa mikono na mazingira kwa ujumla ni muhimu kwa usalama wa afya za wanajamii hasa watoto ili kukabiliana na magonjwa yatokanayo na uchafu katika nchi ya Tanzania na duniani kote.
“Upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira shuleni unasaidia kupunguza pia gharama za huduma za afya, utoro pamoja na kuhakikisha watu wakiwemo watoto wanakuwa na afya bora, uboreshaji huu wa huduma za maji huleta mabadiliko hasa katika
Aidha Jafo amesema anaishukuru WaterAid Tanzania kwa kushirikiana na JICA kwa kuona umuhimu wa kufadhili mradi huo katika halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ili kuhakikisha ubadilishaji tabia endelevu wa masuala ya usafi katika shule 30 na vituo vya afya 15.
Jafo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hususan lengo namba 3 ambalo linalenga kuhakikisha maisha ya watu wenye afya njema na ustawi wa watu wote wa rika zote na lengo namba 6 linalohusu kuhakikisha upatikanaji wa maji salama, usafi wa mazingira na usafi kama hitaji la msingi zaidi la afya na ustawi wa binadamu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti amesema wilaya hiyo bado inahitaji msaada huo zaidi kwani utasaidia kuwaepusha watoto na magonjwa yatokanayo na maji, hivyo kuboresha ufaulu wao.
“Kisarawe kuna ukatili mkubwa wa kijinsia, tukimsaidia mtoto wa kike akapata maji safi na salama kwa urahisi tutakuwa tumeikoa wilaya yetu, hivyo niwaombe WaterAid na JICA kuendelea kutusaidia hasa katika shule za mbali nasi kama serikali tutaendelea kushirikiana nanyi,” amesema Magoti
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga amesema kuwa ujenzi wa vyoo jumuishi, vituo vya kunawia mikono na viunganishi vya maji na vifaa vya kuhifadhia vimebadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya vituo vya kutolea huduma za afya na shule zilizochaguliwa katika Wilaya ya Kisarawe.
Amesema mradi huo umesaidia kuboresha tabia ya unawaji mikono miongoni mwa walengwa pamoja na kukuza uelewa juu ya masuala ya usafi binafsi na usafi wa mazingira katika shule na vituo vya afya vilivyopo kwenye wilaya hiyo ya Kisarawe.