Waziri wa Afya wa Zambia, Elijah Muchima, ametangaza hali ya tahadhari kutokana na vifo vya mbwa wapatao 400 katika mwezi mmoja uliopita, ambavyo vifo hivyo vinadhaniwa kuhusishwa na mahindi yaliyo athiriwa na kemikali, lakini akionya kwamba binadamu wanaweza kuwa hatarini pia.
Mamlaka za afya zimegundua kuwa, nusu ya sampuli 25 za mahindi zilizojaribiwa kutoka katika kampuni za kusaga nafaka, zilikuwa na viwango vya juu vya aflatoxins, ambayo ni kemikali hatari inavyotokana na fangasi.
Aidha Kulingana na tafiti kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), limetambua kuwa aflatoxins zinaweza kusababisha saratani ya ini kwa binadamu. Uchunguzi huu ulianza baada ya kituo cha televisheni cha Diamond TV cha huko Zambia kuripoti vifo vingi vya mbwa, vinavyodhaniwa kusababishwa na chakula cha mbwa kilichotokana na mahindi.
Mamlaka za Afya nchini humo zimechukua sampuli kutoka kampuni 10 za kusaga nafaka ambazo zinahusika na uzalishaji wa chakula cha mbwa na unga wa mahindi, ambao hutumiwa sana na watu nchini Zambia kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Ingawa hakuna vifo vya binadamu vilivyoripotiwa mpaka sasa, hata hivyo Taasisi ya Afya ya Umma ya Zambia inaendelea kuchunguza athari zinazoweza kutokea kwa jamii.
Hata hivyo hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka, huku baadhi ya wananchi wa Zambia wakishangaa kwa nini serikali haijatangaza majina ya bidhaa za unga wa mahindi zilizoathirika.