Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesisitiza ushirikishwaji wa vyuo vya kilimo katika mradi wa Kilimo wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) ili wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo kilimo cha kisasa.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akiweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dkt. Samia Suluhu Hassan – Mlazo/ Ndogowe wakati akiwa ziarani mkoani Dodoma. Amesema ni muhimu kuondoa dhana ya kwamba kilimo hakina faida kuanzia kwa walimu pamoja na wanafunzi wa kilimo kwa kuwashirikisha katika miradi ya kilimo cha kisasa ikiwemo skimu za umwagiliaji.
Amewasihi wanafunzi wa Vyuo vya Kilimo kutumia muda wa likizo katika kushiriki kwenye miradi hiyo.
Makamu wa Rais amesema Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dkt. Samia Suluhu Hassan – Mlazo/ Ndogowe ni mradi muhimu kwa Mkoa wa Dodoma ambao una hazina kubwa ya maji chini ya ardhi. Amesema mradi huo ni suluhisho la kuondokana na tatizo la ukosefu wa chakula cha kutosha
Amewapongeza viongozi na wananchi wa vijiji vya Mlazo na ndogowe kwa kutambua umuhimu wa mradi huo na kutoa ardhi hekari elfu 11 zinazotumika kutekeleza mradi.
Makamu wa Rais amesema Mradi huo utaenda sambamba na ujenzi wa kituo cha afya ili kuwaondolea adha wananchi wa Kijiji cha Mlazo ya kufuata huduma za afya maeneo ya mbali. Aidha ameagiza kufikishwa kwa huduma ya mawasiliano ya simu katika vijiji hivyo.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kutenga mapema maeneo ya malisho na miundombinu ya maji kwaajili ya wafugaji waliopo katika vijiji hivyo ili kuepusha mifugo kuvamia mazao yatakayozalishwa katika mashamba ya BBT.
Pia Makamu wa Rais ameigiza ya Maliasili na utalii kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Chamwino kuhakikisha inapatikana njia ya Wanyama (usharoba) ili kuwaruhusu Wanyama hao waweze kupita.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amesema katika kuendeleza mradi wa Jenga Kesho Iliyobora katika Kilimo, tayari Wizara imetoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kutenga maeneo ya kilimo ambayo yatawekewa miundombinu ya umwagiliaji na kuwawezesha wananchi katika maeneo hayo kuweza kushiriki katika kilimo.
Ameongeza kwamba katika kutoa fursa kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vya Mlazo na Ndogowe unakotekelezwa mradi huo, jumla ya hekari 1000 zimetengwa na zitawekwa miundombinu ya umwagiliaji kwaajili ya wanakijiji ambao wataweza kufanya shughuli za kilimo kwa manufaa yao. Pia amesema hekari 1000 zimetengwa kwaajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dkt. Samia Suluhu Hassan – Mlazo/ Ndogowe unatekelezwa katika Kijiji cha Mlazo Jimbo la Mvumi Wilayani Chamwino ukigharimu shilingi bilioni 20.6
Jumla ya vijana 420 kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania watashiriki katika Mradi huo ambapo vijana 50 ni kutoka vijiji vya Mlazo na Ndogowe.