Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imetoa wito kwa umma kusaidia katika kukamatwa tena kwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware anayeripotiwa kutoroka kutoka kituo cha polisi..
Collins Jumaisi Khalusha anadaiwa kutoroka kutoka mikononi mwa polisi mnamo siku ya Jumanne, Agosti 20, pamoja na washukiwa wengine kumi na wawili. Alikuwa anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Gigiri na aliratibiwa kushtakiwa kwa mauaji.
Katika bango lililotolewa Alhamisi asubuhi, idara ya DCI ilitangaza kuwa zawadi ya pesa taslimu ambayo haijabainishwa itatolewa kwa yeyote ambaye atatoa habari zitakazosaidia kumkamata tena mshukiwa huyo anayetoka kaunti ya Vihiga.
“Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) inaomba usaidizi wa umma katika kutoa taarifa ambazo zinaweza kusaidia kukamatwa tena kwa Collins Jumaisi Khalusha. Alipangiwa kushtakiwa kwa mauaji lakini akatoroka kutoka mikononi mwa polisi mnamo Jumanne 19/8/2024,” bango lililotolewa na DCI lilisomeka.
Ilisomeka zaidi, “Zawadi kubwa ya pesa itatolewa kwa mtu yeyote aliye na habari za kuaminika zitakazopelekea mshukiwa kukamatwa. Mshukiwa anatoka lokesheni ndogo ya Shiru, lokesheni ya Shaviringa, Kaunti Ndogo ya Hamisi katika Kaunti ya Vihiga.”