Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe Dkt.Scolastika Kevela ametoa msaada wa kiti mwendo kwa mhitaji Happy Mtewa mzaliwa wa Malangali wilayani Wanging’ombe ili kuweza kumsaidia kupunguza changamoto ikiwemo kutembea anapohitaji kufika maeneo mbalimbali wakati wa ujasiriamali wake.
Akizungumza mara baada ya kupokea kiti hicho wakati wa ziara ya mwenyekiti wa UWT katika kijiji cha Mtapa Happy Mtewa binti mwenye umri wa miaka ishirini na tano amemshukuru mwenyekiti wa UWT kwa msaada huo huku pia akiomba kusaidiwa mtaji utakaomuwezesha kuongeza wigo wa kazi yake ya ujasiliamali kwenye ushonaji wa vitambaa.
“Ninashukuru sana kwa msaada huu nilioupata lakini pia watu wa Mtapa kwa upendo waliouonesha kwangu,mimi nimepanga Igwachanya ninalipa elfu kumi kwa mwezi,shughuli yangu kubwa ni kushona tu vitambaa mbalimbali vikiwemo vya sofa lakini ninashonea nyumbani nilikuwa ninaomba Mungu akisaidia nipate hata kibanda cha kushinda nikishona vitambaa vyangu”amesema Happy
Naye Mwenyekiti wa UWT anasema pamoja na kutambua jitihada za watu wenye ulemavu wenye uwezo wa kujitaftia kipato kama binti huyo lakini ameamua kufanya tendo la huruma ili kutimiza maandiko.
“Nimeona nifanye tendo la huruma kwasababu vitabu vinaeleza kuwa dini iliyobora ni kuwasaidia wahitaji,wewe Mungu amekujalia kila kitu huoni kwamba mwenzetu kama huyu anahitaji tumsaidie”amesema Dkt.Scolastika Kevela
Baadhi ya viongozi akiwemo diwani wa viti maalum tarafa ya Mdandu Vumilia Kilamlya wametoa shukrani kwa mwenyekiti kwa kuona haja ya kuwasaidia wahitaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe kwa kuwa pia jambo hilo linaimarisha pia chama chao.
Aidha licha ya kutoa msaada huo,wanawake wa UWT Mtapa wameshiriki na kumuunga mkono Mweyekiti wao ambapo katika zoezi la kumkabdishi kiti mwendo mhitaji wamefanikiwa kuchangia kiasi cha zaidi ya laki moja na kumkabidhi binti huyo ili aweze kuongeza mtaji wake wa kushona vitambaa.