Malawi imeanza kuchukua hatua za uchunguzi kwa ajili ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya mpox katika mipaka yote ya kuingilia nchini humo. Hatua hii imechukuliwa siku chache baada ya kuripotiwa kwa kesi mbili zinazoshukiwa kuwa na mpox, ambazo kwa sasa zinangoja majibu ya vipimo vya maabara.
Miongoni mwa walioathirika ni mwanaume mwenye umri wa miaka 31 ambaye anapatiwa matibabu hospitalini, na kijana wa miaka 17 ambaye anapata matibabu akiwa nyumbani.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imekuwa kitovu cha aina hatari zaidi ya virusi vya mpox ambavyo vilianza mwaka jana na kuenea katika zaidi ya mataifa kumi ya Afrika. Wiki moja iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hali ya dharura ya kiafya kuhusu kuenea kwa aina mpya ya mpox.
Shirika la Afya ya Umma la Afrika limesema kuwa baadhi ya nchi barani humo zitaanza kutoa chanjo dhidi ya mpox katika siku chache zijazo. Hata hivyo, nchini Malawi, mpango wa chanjo hautawalenga watu wote kama ilivyokuwa kwa chanjo ya Covid-19, bali utalenga watu walio katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa.
Adrian Chikumbe, msemaji wa Wizara ya Afya ya Malawi, amesema kuwa hatua ya kuwapima wageni ni sehemu ya mikakati ya kuzuia kusambaa kwa mpox, ikiwemo kampeni za uhamasishaji kupitia mitandao ya afya ya jamii.
Malawi pia imeanzisha kitengo cha uchunguzi wa magonjwa cha kusafiri katika hospitali moja iliyopo mji mkuu wa Lilongwe.
Mtoa huduma wa afya ya jamii, Carol Luka, amewashauri wananchi kuwa na tahadhari kwa kuepuka kugusa watu au vifaa vilivyotumiwa na mtu anayeonyesha dalili za mpox.