Shirika la afya la Umoja wa Mataifa Jumatatu lilizindua mpango wa miezi sita wa kusaidia kukomesha milipuko ya maambukizi ya mpox.
Mpango huo unajumuisha kuongeza wafanyikazi katika nchi zilizoathirika na kuongeza mikakati ya ufuatiliaji, kuzuia na kukabiliana.
Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema linatarajia mpango huo kuanzia Septemba hadi Februari mwaka ujao utahitaji ufadhili wa dola milioni 135 na unalenga kuboresha ufikiaji wa haki wa chanjo, haswa katika nchi za Kiafrika zilizoathiriwa zaidi na mlipuko huo.
“Milipuko ya mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi jirani inaweza kudhibitiwa, na inaweza kukomeshwa,” Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus katika taarifa yake.
Shirika hilo “linaongeza kwa kiasi kikubwa wafanyikazi” katika nchi zilizoathirika, ilisema. Katikati ya Agosti, WHO iliainisha mlipuko wa sasa wa mpox kama dharura ya afya ya kimataifa.
Jumatatu pia, msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit alisema Ujerumani inatoa dozi 100,000 za chanjo ya mpox kwa nchi zilizoathirika kutokana na hisa zinazoshikiliwa na jeshi lake, shirika la habari la Ujerumani dpa liliripoti.