Kifo cha mhamiaji aliyezuiliwa katika eneo lililozuiliwa la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guarulhos, katika eneo la mji mkuu wa São Paulo, kimeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa haki za binadamu.
Eneo hilo kwa mara nyingine tena ni eneo la mgogoro kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kukidhi mtiririko wa wahamaji nchini humo.
Mhamiaji huyo mwenye umri wa miaka 39 kifo chake kilitokea tarehe 13 Agosti baada ya kupatiwa huduma ya matibabu uwanjani hapo, ingawa chanzo halisi cha kifo hicho bado hakijafahamika.
Mhamiaji huyo alikuwa miongoni mwa kundi la wasafiri wasiokubalika waliokuwa wakishikiliwa kwenye eneo maalumu la uwanja wa ndege kutokana na ukosefu wa nyaraka au visa vinavyohitajika ili kuingia nchini Brazil, kulingana na ripoti ya Reuters.
Watu hao wamewekwa katika eneo lenye upungufu wa huduma muhimu kama vile chakula, maji, na sehemu za kuoga. Ofisi ya Watetezi wa Umma ya Brazil imekosoa hali hiyo, ikieleza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, huku afya za walioko kizuizini zikiendelea kuzorota.
Tukio hili linakuja wakati ambapo serikali ya Brazil inajiandaa kutekeleza kanuni kali zaidi za kuingia nchini humo, kwa lengo la kuzuia wahamiaji kutumia nchi hiyo kama kituo cha mpito kuelekea Marekani na Canada.