Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani Bruno Labbadia ameteuliwa kuwa kocha mpya wa Nigeria, ikiwa ni uteuzi wa tatu wa wadhifa huo mwaka huu.
Shirikisho la Soka la Nigeria lilitoa tangazo hilo kwenye mtandao wa kijamii siku ya Jumanne, likisema uteuzi wake “ulifanyika mara moja” lakini bila kutoa maelezo yoyote ya muda wa mkataba.
Labbadia anachukua uongozi siku 12 kabla ya Nigeria kuanza kampeni ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 kwa mechi ya Kundi D dhidi ya majirani zao Benin mjini Uyo.
Timu hiyo pia itacheza ugenini nchini Rwanda siku tatu baadaye. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 58, ni kocha wa muda wa Bundesliga ambaye amewahi kuinoa Bayer Leverkusen, Hamburg, VfB Stuttgart, VfL Wolfsburg na Hertha Berlin.
Hii itakuwa kazi yake ya kwanza nje ya Ujerumani anachukua nafasi ya Finidi George, ambaye aliongoza mechi nne mapema mwaka huu.