Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezisihi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuongeza ushirikiano katika ufanisi wa kazi zao.
Dk. Mwinyi alitoa nasaha hizo Ikulu, Zanzibar, alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Ndugu. Crispin Francis Chalamila, aliyekwenda kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.
Rais Dk. Mwinyi amezishauri taasisi hizo mbili kuzidisha ushirikiano hasa kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo kwa maslahi ya taifa.
Naye Ndugu. Chalamila amemuahidi Rais Dk. Mwinyi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya ZAECA na TAKUKURU kufanikisha majukumu ya taasisi hizo.
Vilevile, Bw. Chalamila amesifu na kupongeza juhudi za maendeleo makubwa zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.
Amesema, mbali na majukumu mengine waliyonayo, TAKUKURU na ZAECA imekuwa rahisi kwao kushirikiana, hasa kudhibiti wahalifu wa pande mbili za Muungano wanaojaribu kukimbilia mipaka ya Bara na Zanzibar.