Shirika la Umoja wa Mataifa limeahirisha usafirishaji misaada kwenda Gaza kwa muda baada ya jeshi la Israeli kutoa maagizo mapya ya kuhamasisha uhamishaji.
Maagizo haya yameathiri mpango wa kampeni ya chanjo ya polio inayokusudia kufikia watoto zaidi ya 640,000 katika eneo hilo.
Jeshi la Israeli lilitoa maagizo ya kuwahamisha wapalestina katika maeneo ya Deir Al-Balah, katikati ya Gaza hali iliyowalazimu wakimbizi wa Kipalestina kuhama tena, huku Umoja wa Mataifa ukikabiliwa na changamoto katika kutekeleza kampeni ya chanjo.
Hivi karibuni, Gaza ilithibitisha kisa cha kwanza cha polio kwa miaka 25, kwa mtoto wa miezi kumi ambaye hakuwa amechanjwa.
Polio ni ugonjwa unaosambaa kwa haraka na unaweza kusababisha ulemavu au kifo.
Jumatatu, shirika la COGAT la Israel lilisema kuwa zaidi ya dozi 1.2 milioni za chanjo zilifika Gaza kupitia kivuko cha Kerem Shalon, na kampeni ya chanjo itaendeshwa kwa ushirikiano na Jeshi la Ulinzi la Israeli.
Hata hivyo, kwa sasa hakuna usafirishaji wa misaada unaoendelea.
UNRWA na Wizara ya Afya ya Palestina walisisitiza kuwa maandalizi ya kampeni ya chanjo yanaendelea, huku juhudi zikifanywa kutoa dozi ziada 400,000 ili kuchanja asilimia 95 ya watoto wa chini ya miaka 10.
Afisa wa UN alisema kuwa operesheni za UN hazitaondoka Gaza, lakini inahitaji kutafuta mahali mapya kufuatia maagizo mapya ya uhamishaji.