KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg.Ally Salum Hapi MNEC) amepongeza Uongozi wa CCM na Serikali ya Wilaya ya Wanging’ombe kwa kuwa na ushirikiano wa kutosha kuhakikisha Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025 inatekelezwa kwa vitendo wilayani hapo.
Ameyasema hayo leo Tarehe 27/08/2024 baada ya kuwasili katika ofisi za CCM za Wilaya ya Wanging’ombe kusomewa taarifa ya Chama, Jumuiya ya Wazazi na Serikali na kuona ushirikiano mkubwa walionao.
Aidha amewasisitiza viongozi wa chama na jumuiya zake kuhakikisha kamati za ushindi za chama hicho za kata, matawi na shina zinatekeleza majukumu yake na kuleta taarifa ya kazi zao na kuzifanyia kazi kwa maslahi mapana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amewahimiza viongozi kutoa elimu ya wanachama wa CCM na jumuiya zake pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura na daftari la makazi ili wapate haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani 2025.
“Nawasihi viongozi wa CCM kuendelea kutoa elimu kwa wanachama wetu na wananchi juu ya kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura na daftari la makazi ili wapate nafasi na haki ya kupiga kura muda ukifika wa uchaguzi wa serikali za Vijiji Vitongoji na Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu;
“Mwaka huu kuna uchaguzi wa serikali za mitaa ni wajibu wenu viongozi wa CCM na Jumuiya ya Wazazi, UWT na UVCCM kuwashawishi wanachama wetu ambao mnaona wanatosha wana sifa kushika nafasi hizi za serikali za mitaa kwa maslahi mapana ya chama na wananchi siyo mtu umshawishi mtu ambae anayefaa kwa maslahi ya tumbo lako hiyo tuseme hapana” alisema Hapi.