Taasisi ya THT innovation Ltd (THT) iliyojijengea umaarufu katika kukuza vipaji na kutoa mafunzo katika sekta ya sanaa nchini Tanzania imeungana na msanii maarufu nchini Mwasiti Almas kuwawezesha mabinti walioko kwenye sanaa kupitia programu ya ‘Kipepeo Mweusi’. Programu hii imefanyika wiki iliyopita kupitia warsha ya mafunzo ikiwahusisha mabinti walioko kwenye Sanaa za muziki, uigizaji na kucheza ambao wamejifunza namna mbalimbali ya kukabiliana na changamoto zilizoko kwenye soko la Sanaa nchini Tanzania.
Kupitia mradi huu zaidi ya mabinti 200 wanaofanya sanaa za muziki, kucheza na uigizaji wamepata mafunzo mbalimbali na kuwawezesha kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika Sanaa.
Katika warsha iliyofanyika viwanja vya THT Mikocheni,Muanzilishi wa KipepeoMweusi Mwasiti Almas amesema warsha hii imekuwa na matokeo makubwa kwa sababu kumekuwa na mwitikio mkubwa wa mabinti na wadau.
“Naona fahari kuungana na wadau kuwasaidia mabinti. Kupitia mradi huu wa kipepeo mweusi tunahamasisha mabinti kusimamia misingi mikuu minne; Kuwa tofauti, kuwa mtu wa malengo, Uthubutu, na kuwa na ndoto kubwa” alisema Mwasiti