Zaidi ya Wanigeria milioni 31.8 waripotiwa kukosa chakula kutokana na changamoto za kiusalama na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, serikali ilisema Jumanne, ikitoa mfano wa utafiti uliofanywa na washirika kadhaa wa maendeleo wa kimataifa wa nchi hiyo.
Kiwango cha uhaba huo, ambacho kimesababisha utapiamlo miongoni mwa wanawake na watoto, kilielezwa na washirika hao wa maendeleo katika mkutano na serikali siku ya Jumatatu na Jumanne, wizara ya bajeti na mipango ya uchumi ilisema katika taarifa yake.
Matokeo hayo yanaonyesha kuongezeka kwa kasi kutoka kwa watu milioni 18.6 waliotathminiwa kama hatari ya uhaba mkubwa wa chakula kutoka Oktoba hadi Desemba 2023 na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa.
“Ongezeko la bei za bidhaa za chakula, ambalo linatokana na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta pamoja na changamoto za kiusalama, kumeweka mamilioni ya Wanigeria katika hali mbaya,” wizara ilisema.