Jeshi la Israel limeanzisha operesheni kubwa katika miji minne ya Ukingo wa magharibi mapema leo hii, huku likiendelea na vita vyake vya miezi kumi dhidi ya Gaza.
Hali ya ghasia imeongezeka katika Ukingo wa Magharibi kutokana na mzozo ulioanzishwa na mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7.
Vita hivyo vimepoteza zaidi ya watu 40,000 huko Gaza, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo. Operesheni ya Israeli, iliyohusisha mashambulizi ya anga, vikosi vya ardhini, na buldoza, ilidaiwa kusababisha vifo vya watu angalau kumi, kwa mujibu wa Kamati ya Msalaba Mwekundu ya Kipalestina. Miji iliyoshambuliwa ni Jenin, Nablus, Tubas, na Tulkarem, ambapo walengwa walikuwa na mashambulizi kwenye magari na kambi za wakimbizi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli, Israel Katz, alisema jeshi linafanya kazi kwa nguvu kuondoa miundombinu ya kigaidi inayodaiwa kuwa ya Kundi kutoka Iran.
Hii ni katika juhudi za kukabiliana na vitisho vinavyotokana na Iran, mpinzani mkuu wa Israel katika eneo hilo. Operesheni hii mpya inakuja baada ya mashambulizi ya anga yaliyosababisha vifo vya watu watano katika Ukingo wa magharibi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, tangu mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7, wapalestina zaidi ya 650 wameuawa na vikosi vya Israel au walowezi, huku Waisraeli 19 wakipoteza maisha kutokana na mashambulizi ya wapalestina. Operesheni hizi zimekuwa za mara kwa mara lakini ni nadra kufanywa katika miji mingi kwa wakati mmoja.