Shirika la afya la Umoja wa Afrika limesema hapo jana kuwa linakaribia kupata karibu dozi milioni moja za chanjo ya ugonjwa wa homa ya nyani.
Shirika hilo limetaka makampuni kubadilishana teknolojia ya kutengeneza chanjo ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (CDC) Jean Kaseya alipokuwa akihutubia mkutano wa kikanda wa Shirika la Afya Duniani WHO mjini Brazzaville nchini Jamhuri ya Congo.
Nchi kadhaa zimeahidi kupeleka chanjo katika nchi za Kiafrika zilizokumbwa na miripuko ya Mpox, huku Uhispania pekee ikiahidi dozi 500,000 za chanjo. WHO ilitangaza dharura ya afya ya kimataifa mapema mwezi huu kutokana na kuenea kwa maambukizi ya homa ya nyani.