Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kusitisha harakati za wafanyakazi wake katika Ukanda wa Gaza hadi itakapotangazwa tena baada ya moja ya magari yake kushambuliwa kwa risasi karibu na kituo cha ukaguzi kinachodhibitiwa na Israeli.
Tukio hilo lilitokea Jumanne usiku wakati gari hilo lilipokuwa likikaribia kituo cha ukaguzi cha Wadi ya Gaza Bridge. WFP imesema kuwa hakuna mfanyakazi yeyote aliyekuwemo ndani ya gari hilo aliyedhurika kimwili.
Msemaji na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Stephane Dujarric, wameilaumu Israeli kwa shambulio hilo, wakisema kuwa gari hilo la kibinadamu, lililoonekana wazi, lilipigwa risasi mara 10 na wanajeshi wa Israeli, huku risasi zikielekezwa kwenye madirisha ya mbele ya gari, ikiwemo upande wa dereva.
Msafara huo ulikuwa ukirudi kutoka kwenye misafara ya kutoa msaada ya Karem Abu Salem, na harakati zao zilikuwa zimepangwa kwa ushirikiano na jeshi la Israeli. Dujarric aliongeza kuwa tukio hilo linaonesha kuwa mfumo wa uratibu wa usalama hautekelezwi ipasavyo, na kwamba juhudi za kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii zinaendelea.
Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cindy McCain, alilaani shambulio hilo na kusema kuwa ni tukio lisilokubalika, na kwamba ni sehemu ya matukio ya kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wa shirika hilo huko Gaza. WFP imeitaka mamlaka ya Israeli na pande zote zinazohusika kwenye mzozo huo kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wote wa misaada huko Gaza.
WFP iliongeza kuwa, ingawa hii sio mara ya kwanza kwa timu yake kukumbana na hali ya hatari katika vita hivi, ni mara ya kwanza kwa gari lake kushambuliwa moja kwa moja licha ya kuwa na vibali vinavyohitajika.