Wizara ya afya nchini Burundi inasema watu 193 wamelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa ugonjwa wa Mpox na sasa inaomba msaada wa kifedha ili kupambana na msambao wa ugonjwa huo.
Serikali ya Burundi inasema, inatafuta karibu Dola Milioni 1 kupambana na maambukizi yanayoendelea kuongezeka nchini humo.
Wizara ya afya inasema watu 231 wameambukizwa na ugonjwa huo kufikia Agosti tarehe 25, wengine 38 wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani na hakuna aliyepoteza maisha.
Wilaya 29 kati ya 49 zimeripoti maambukizi ya ugonjwa huo, kwenye nchi hiyo inayokabiliwa na changamoto ya miundo mbinu za kisasa za kiafya kukabiliana na mlipuko wa magonjwa kama Mpox.
Wataalam wa afya wanasema elimu inapaswa kutolewa kwa watu wanaokutana kwenye maeneo ya umma kama masoko, makanisa na shuleni ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.