Maelfu ya Waisraeli walijitokeza mitaani Jumapili usiku baada ya mateka sita zaidi kupatikana wakiwa wamekufa huko Gaza. Waandamanaji walikusanyika wakimtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas ili kuwarejesha mateka waliobaki nyumbani.
Haya yamekuwa maandamano makubwa zaidi tangu vita kuanza, huku Shirikisho la Wafanyakazi la Israel likitangaza mgomo wa jumla Jumatatu, lengo likiwa ni kuvuruga sekta kuu za uchumi kama benki na huduma za afya,mgomo huu ni wa kwanza tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7.
Wengi wanamlaumu Netanyahu kwa kushindwa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, ingawa baadhi wanamuunga mkono kwa mkakati wake wa kuendelea na vita mpaka kushinda kabisa dhidi ya Hamas. Mazungumzo ya kusitisha mapigano yamekuwa yakisuasua kwa miezi kadhaa, na hali hii imezidisha hasira kwa wananchi.
Aidha Mateka watatu waliopatikana wamekufa walitarajiwa kuachiliwa awamu ya kwanza ya makubaliano yaliyopendekezwa Julai, jambo lililoibua hasira zaidi. Jeshi la Israel lilisema mateka hao waliuawa kabla vikosi vyao kufika kwenye eneo la tukio, na wakalaumu Hamas kwa kushindwa kufikia makubaliano.
Mmoja wa mateka hao ni Hersh Goldberg-Polin, raia wa Marekani mwenye asili ya Israel, ambaye alionekana katika video iliyotolewa na Hamas mwezi Aprili, akionyesha kuwa bado yuko hai. Hii ilisababisha maandamano makubwa nchini Israel.
Hamas imetoa pendekezo la kuachilia mateka kwa sharti la kumalizika kwa vita, kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka Gaza, na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina. Hata hivyo, hali ya hasira na huzuni inaendelea kukua miongoni mwa Waisraeli huku mazishi ya mateka yakiendelea kufanyika.