Klabu ya Arsenal imekataa rasmi ofa ya €35 milioni iliyotolewa na Al Ittihad ya Saudi Arabia kwa ajili ya kumchukua winga Leandro Trossard. Ofa hiyo ilitolewa kabla ya dirisha la usajili la Saudi Pro League kufungwa, huku Al Ittihad wakiwa wanatafuta winga mpya wa kuimarisha kikosi chao.
Trossard, ambaye amekuwa mchezaji muhimu chini ya kocha Mikel Arteta, anachukuliwa kama sehemu muhimu ya mfumo wa mzunguko wa wachezaji wa Arsenal. Arsenal wamesisitiza kwamba Trossard hayupo sokoni na ni mchezaji muhimu kwa mipango yao ya msimu huu.
Katika hatua nyingine, Al Ittihad inakaribia kukamilisha usajili wa Danilo Pereira kutoka Paris Saint-Germain, ambapo mchakato wa dili hilo uko asilimia 90 kukamilika. Pia, klabu hiyo sasa inafanya mazungumzo na FC Porto kwa ajili ya kumsajili winga wa Kibrazil, Galeno, ambapo tayari wametuma ofa rasmi.