Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama, Jacquemain Shabani, ametangaza idadi ya vifo vya watu 129 kufuatia jaribio la kutoroka katika gereza la Makala lililopo jijini Kinshasa siku ya Jumatatu Septemba 2.
Ripoti hii ya muda imetolewa kufuatia mkutano wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani.
Idadi ya muda inafikia vifo 129, ikiwa ni pamoja na watu 24 waliouawa kwa risasi baada ya onyo, waathiriwa wengine walifariki kwa kusukumwa au kukosa hewa. Pia kuna majeruhi 59 wanaohudumiwa na Serikali, pamoja na kesi chache za wanawake kubakwa,” amebainisha Jacquemain Shabani, kulingana na Radio OKAPI.
Tume iliyoundwa kwa ajili ya uchunguzi imebaini majeruhi 59 ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu na Serikali ili kupata huduma stahiki, anaongeza Waziri wa Mambo ya Ndani.
Jacquemain Shabani ameongeza kuwa hali imerejea kuwa shwari katika gereza hilo na kwamba uchunguzi unaendelea.