Msemaji wa mrengo wa kijeshi wa Hamas, Brigedi za Al-Qassam, Abu Obaida, alitangaza Jumatatu kwamba kundi hilo limetoa maagizo mapya kwa walinzi juu ya jinsi ya kushughulikia mateka ikiwa vikosi vya Israeli vinakaribia maeneo yao huko Gaza, Reuters inaripoti.
Siku ya Jumapili, jeshi la Israel liliripoti kupatikana kwa miili sita ya mateka kutoka kwenye handaki katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza, wakidai kuwa Hamas ndio waliohusika na vifo vyao. Obaida alisema kundi lake linaishikilia Israel kuhusika na vifo hivyo.
Alisema maagizo hayo mapya, ambayo hakueleza kwa kina, yalitolewa kwa walinzi wa mateka baada ya operesheni ya uokoaji ya Israel mwezi Juni. Wakati huo, wanajeshi wa Israel waliwaachilia mateka wanne katika shambulio baya ambalo mamia ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto waliuawa.
“Msisitizo wa Netanyahu wa kuwaachilia wafungwa kwa shinikizo la kijeshi, badala ya kufunga makubaliano inamaanisha watarejeshwa kwa familia zao katika sanda. Familia zao lazima zichague ikiwa wanataka wafu au wawe hai,” akasema.