Ajali mbaya imetokea asubuhi ya leo hii katika mji wa Tai an, mkoa wa Shandong, mashariki mwa China, ambapo basi lililokuwa limebeba wanafunzi limepoteza mwelekeo na kugonga kundi la wanafunzi na wazazi waliokuwa wakisubiri kuingia shule. Polisi na vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kuwa watu 11 wamepoteza maisha na wengine 13 wamejeruhiwa.
Basi hilo, ambalo lilikuwa maalum kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi, lilipoteza udhibiti lilipokuwa likielekea kwenye makutano ya barabara na kisha kugonga kundi la watu waliokuwa wakisubiri nje ya lango la shule ya sekondari. Wanafunzi watano na wazazi sita walifariki dunia katika ajali hiyo.
Dereva wa basi amekamatwa na uchunguzi wa kina kuhusiana na ajali hii unaendelea. Mmoja wa majeruhi yupo katika hali mbaya, wakati wengine wakiwa katika hali ya utulivu.
China imekumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya magari na visa vya kuchomwa visu dhidi ya watoto wa shule katika miaka ya hivi karibuni, pamoja na ajali mbaya za barabarani zinazohusisha mabasi ya shule.