Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amebainisha kuwa uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Indonesia umekuwa maradufu ikizingatiwa ongezeko la thamani ya mauzo ya nje kutoka Tanzania kwenda Indonesia kwa wastani wa dola za Marekani milioni 13.53 mwaka 2019 hadi dola milioni 33.77 mwaka 2023.
Bidhaa kuu za Tanzania zinazouzwa nchini Indonesia ni pamoja na tumbaku, kakao, maharage, karanga, karafuu, pamba, na mafuta ya mawese.
Rais Dk. Mwinyi ameeleza kwa furaha kuwa Tanzania na Indonesia zinaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kwa mwaka huu 2024 pia, ameongeza kuwa ni jambo la fahari kwa nchi hizo mbili kujivunia urafiki uliodumu na unaoendelea kukua siku hadi siku.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika mwendelezo wa siku ya pili ya Jukwaa la Indonesia na Afrika 2024, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano, hoteli ya Mulia, Bali, Indonesia.
Dk. Mwinyi katika jukwaa hilo amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tanzania bado ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo kilimo, madini, utalii, na uchimbaji wa mafuta na gesi na uchumi wa buluu hivyo, Rais Dk. Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia kuja Tanzania Bara na Zanzibar kuzifanyia kazi fursa hizo.
Kwa upande wa elimu, Rais Dk. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Indonesia kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya maendeleo ya rasilimali watu kupitia udhamini wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika nyanja mbalimbali.
Rais Dk. Mwinyi ameishawishi Serikali ya Indonesia iongeze udhamini wa masomo pamoja na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali kama vile huduma za Afya na Sayansi ya Tiba, Uhandisi, ICT, Uvuvi, Utalii, Ufugaji wa Samaki, na Kilimo.
Wakati huo huo Rais Dk. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini (MoU) wa Makubaliano ya udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa lengo la ushirikiano katika usajili wa bidhaa hizo, ukaguzi pamoja na kupeana taarifa za madhara ya dawa na vifaa tiba kwenye masoko.
Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika pembezoni mwa ukumbi mkuu wa mikutano katika hoteli ya Mulia ambapo kwa upande wa Tanzania amesaini Mkurugenzi Mkuu Dkt. Adam Fimbo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi Tanzania (TMDA), na kwa niaba ya Serikali ya Indonesia amesaini Mwenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Chakula Indonesia (BPOM) Dkt. Taruna Ikrar.
Rais Dk. Mwinyi pia alipata fursa ya kutembelea maonesho ya biashara ndani ya hoteli ya Mulia kutoka nchi washiriki wa Jukwaa la Indonesia na Afrika 2024 ikiwemo Tanzania.