Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ameripotiwa kuamuru kuuawa kwa maafisa wapatao 30 kufuatia kushindwa kwao kuzuia mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yaliyosababisha vifo vya watu takriban 1,000 mwezi Julai.
Kulingana na ripoti ya Chosun TV ya Korea Kusini , ilimnukuu kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un kutaka adhabu kali itolewe kwa wale wanaodaiwa kuhusika na hasara isiyokubalika ya maisha ya watu, iliyosababishwa na mafuriko ya hivi majuzi.
Mafuriko hayo, ambayo yaliharibu zaidi ya nyumba 4,000 na kuwahamisha wakazi 15,000, yalisababisha Kim Jong Un kutoa agizo la adhabu kali kwa maafisa waliohusika. Ingawa majina ya maafisa walionyongwa hayajatajwa, Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA) liliripoti kwamba Kang Bong-hoon, katibu wa Kamati ya Chama ya Mkoa wa Chagang tangu 2019, alikuwa miongoni mwa viongozi walioondolewa kwenye nyadhifa zao na Kim Jong- un.
Kim Jong Un pia alitembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko na kusema kuwa itachukua miezi kadhaa kujenga upya na kurejesha maeneo hayo. Serikali ilitoa makazi kwa watu 15,400 mjini Pyongyang, wakiwemo vikundi vya watu walio katika mazingira magumu kama vile watoto, wazee, na askari walemavu.
Hata hivyo, Kim alikanusha ripoti za vifo vingi kutokana na mafuriko hayo, akizitaja kama uvumi wa uongo uliosambazwa na Korea Kusini kama sehemu ya kampeni ya kuharibu sifa ya Korea Kaskazini kimataifa. Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa idadi ya adhabu za kifo nchini Korea Kaskazini imeongezeka sana tangu janga la COVID-19, kutoka wastani wa 10 kwa mwaka kabla ya janga hadi takriban 100 kwa mwaka.