Wizara ya Afya ya Palestina imethibitisha kuwasili Shehena mpya ya chanjo za polio, jumla ya dozi 350,000, huko Gaza.
Chanjo hizi zimefika wakati ambapo kampeni ya chanjo inaendelea huku vita vya Israel dhidi ya Gaza vikiwa vinaendelea kwa siku ya 334, vikiua zaidi ya Wapalestina 40,819, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi zaidi ya 94,291.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Palestina, Majed Abu Ramadan, chanjo hizo zimehifadhiwa katika maghala ya wizara huko Deir al-Balah baada ya kuwasili Jumanne jioni. Alisema kuwa hatua hizi zimefanyika kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Aidha Waziri huyo aliongeza kuwa kwa kuwasili kwa shehena hii ya pili, idadi ya jumla ya dozi za chanjo zilizopokelewa Gaza sasa inafikia takriban milioni 1.6, kiasi ambacho kinatosha kuwachanja watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 10 kwa dozi mbili za chanjo ya polio.